Shirika la Habari la Hawza | Huenda ukajiuliza swali hili mwenyewe: kwa nini dunia yetu ambayo inapaswa kuwa imejaa upendo na huruma imejaa dhuluma na uonevu? Mwanadamu ataendelea kushuhudia hadi lini haya yote, ukosefu wa haki na ubaguzi?
Kwa nini baadhi ya watu, kwa sababu ya dhuluma ya madhalimu, wanaishi katika umasikini wa kupindukia kiasi kwamba hawawezi hata kukidhi mahitaji yao ya msingi ya maisha? Kwa nini baadhi ya watu wanadhulumiwa kwa sababu tu ya rangi ya ngozi zao? Kwa nini tushuhudie watoto ambao mifupa yao inaonekana kwa sababu ya njaa? Hadi lini tutashuhudia nyumba za watu wasio na hatia zikiharibiwa kwa mabomu ya ndege za kivita? Hadi lini tutashuhudia akina baba na kina mama wakiwa wamewabeba watoto wao wasio na hatia, waliotapakaa damu mikononi mwao?
Kwa nguvu ya nani na matumaini ya nani matatizo haya yatatatuliwa? Ni nani atakae wawajibisha wahusika wa jinai hizi zote na ukosefu huu wa haki? Ni katika mahakama ipi duniani ambapo haki ya hawa wanyonge itapatikana?
Haya Na maswali mengine mengi yanayoshughulisha akili ya kila mwanadamu huru.
Lakini pia kuna maswali mengine yasiyohusiana moja kwa moja na dunia hii, ambayo yanaweza kuishughulisha sana akili ya mwanadamu mwenye tafakuri.
Kwa mfano, hadithi ya haya maisha ni ipi? Uhusiano wa Mungu ambaye ameviweka vipengele vya ulimwengu huu wa ajabu na mgumu kwa mpangilio huu makini, na ambaye ameweka jukumu maalumu kwa kila kimoja kati yao, na mimi mwanadamu ukoje? Kwa kifupi, kuhusu namna ya kuongozwa kwangu na uhusiano huo, haiwezekani kuwa nibkwa kughafilika au kutojali.
Maswali haya si maswali ambayo mtu anaweza kuyapuuza kwa urahisi; kwa sababu sisi kama wanadamu tumepewa neema ya akili. Akili inayotulazimisha kufikiri, na ni jambo baya kiasi gani iwapo maisha ya mwanadamu yatatawaliwa na matamanio ya kinyama na kihisia, kiasi kwamba ufalme wa nafsi yake ukose nuru ya akili na fikra. Ni hasara gani kubwa na ya kushangaza!
Maudhui na maswali yaliyotajwa, yanaweza kuwa ni msukumo wa kutufanya tutafute, na kutafuta kitu au mtu atakayekuwa jawabu la maswali yetu na tiba ya maumivu yetu.
Na hiki ndicho kinachojulikana kama “tumaini”. Tumaini la uongofu, tumaini la ukombozi, tumaini la mustakabali uliojaa nuru.
Tumaini na ukombozi unaojitokeza kwa sura ya “Mkombozi”, kwa sura ya “Kiongozi na Mwongozaji”. Mkombozi na Mwongozaji ambaye dini zote zimetabiri kuja kwake.
Myahudi, Mkristo, Mwislamu, Mzartusht, Mhindu, Mbuddha, na hata wale wasiofuata dini yoyote, nao pia wanaamini kuwa kuja kwa mkombozi ni miongoni mwa imani zisizoweza kutengwa na wao. Imani ambayo, katika nyakati za shida na matatizo, huwa ni chanzo cha utulivu kwao na tiba kwa huzuni na maumivu yao.
Utajo wa kuja kwa Mkombozi katika Uislamu
Katika dini ya Uislamu na katika madhehebu ya Kishia, pia kumetajwa sana kuja kwake. Mtu ambaye atakuja na kuijaza dunia iliyojaa dhuluma na uonevu kwa uadilifu na haki. Mtu ambaye atakuwa tumaini la wanyonge wa dunia na adui wa madhalimu na wadhulumu. Mtu ambaye kwa kudhihiri kwake, Mwenyezi Mungu atakamilisha fadhila zake juu ya waja wake. Tofauti ikiwa kwamba kwa mujibu wa imani ya Mashia, mkombozi wa ulimwengu wa wanadamu kwa sasa anaishi miongoni mwa watu, bila kujulikana, hadi wakati ambapo Mwenyezi Mungu Mtukufu atamruhusu ajitambulishe na adhihirike. Hivyo basi, kwa mujibu wa imani ya Mashia, kudhihiri humaanisha kujulikana kwa mkombozi.
Utafiti huu unaendelea…
Maoni yako